Alex Massawe
Posted
Alhamisi,Julai11
2013
saa
9:31 AM
Kwa ufupi
Mkuu wa la Shirika la Polisi la Kimataifa
(Interpol), Tawi la Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Gustav
Babile aliliambia gazeti hili jana kwamba Massawe alikamatwa kati ya
Juni 20 na 25 mwaka huu kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai
akitokea Afrika Kusini.
Dar es Salaam. Mfanyabiashara maarufu nchini,
Alex Massawe ambaye alikuwa anatafutwa na Polisi wa Tanzania kwa muda
mrefu, amekatwa Dubai, Falme za Kiarabu (UAE).
Mkuu wa la Shirika la Polisi la Kimataifa
(Interpol), Tawi la Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Gustav
Babile aliliambia gazeti hili jana kwamba Massawe alikamatwa kati ya
Juni 20 na 25 mwaka huu kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai
akitokea Afrika Kusini.
Babile alisema hivi sasa walikuwa wanaandaa taratibu za kumrudisha nchini ambako amekuwa akisakwa kwa muda mrefu.
“Ombi la kuleta mhalifu nchini kutoka nje ya nchi
(extradition request), lina hatua ndefu. Unajua kuna mlolongo wa
taratibu za kutekeleza ili Massawe aletwe. Kwanza lazima Polisi wa
Tanzania watoe tangazo kwa Interpol kuhusu kumsaka mtu huyo ili aletwe,”
alisema Babile.
Alisema Massawe alikamatwa wakati akifanya taratibu za ukaguzi baada ya kuwasili UAE.
Habari zilizofikia gazeti hili mapema kutoka Dubai
zilieleza kuwa Massawe alikamatwa na maofisa wa usalama wa UAE kutokana
na alama zake za vidole na kuonyesha kuwa alikuwamo kwenye orodha ya
watu waliokuwa wanasakwa na Interpol.
Massawe ambaye anamiliki majumba na biashara ya
utalii katika Miji ya Arusha, Dar es Salaam na Moshi, inadaiwa kwamba
alikutwa na pasi tatu bandia za kusafiria zilizokuwa na majina tofauti
wakati alama zake za vidole zilionyesha anaitwa Alex Massawe.
“Maofisa wa Usalama wa uwanja wa ndege walimuuliza
kuwa wewe ndiye Alex Massawe? Alikana lakini alielezwa kuwa alama za
vidole vinaonyesha anaitwa hivyo,” kilidokeza chanzo cha habari hizi kwa
simu kutoka Dubai. Hata hivyo, Babile alisema hakuwa na taarifa za
Massawe kukutwa na pasi bandia za kusafiria.
Uvumi wa Aprili
Mapema Aprili 27, mwaka huu kulikuwa na habari
kwamba Massawe amekamatwa katika mji mmojawapo ulioko katika Pwani ya
Afrika Kusini.
Habari hizo za kukamatwa kwa Massawe, ambaye pia
hufadhili masuala ya kisiasa na michezo, zilisambaa kupitia mitandao
mbalimbali ya kijamii ya Facebook, Twitter na Jamii Forum. Kulikuwa kuna
mkanganyiko wa taarifa huku wengine wakidai alinaswa akiwa ndani ya
boti huko Afrika Kusini, wengine wakidai alikamatwa wakati akijaribu
kuingia Msumbiji akitokea Malawi.
Akizungumzia hilo Babile alisema huo ulikuwa ni
uzushi na baada ya kuzisikia taarifa hizo walifuatilia katika maeneo
aliyohusishwa kukamatwa na kubaini kwamba hapakuwa na ukweli wowote.